Mungu yupo tayari kutua katika maisha ya mwamini lakini Mungu hatui hovyo, lazima kuwe na mazingira yanayomwezesha kutua ambayo mtu mwamini anapaswa kuwa ameyaandaa.
MAZINGIRA MATANO YA KIUNGU YATAKAYOLETA MGEUKO WA KIUNGU
1. Nguvu za kiungu za kuleta mgeuko tayari zipo lakini lazima awepo mtu wa kuzitumia ili zitende kazi.
Mungu ana nguvu zote za uponyaji, za kusababisha maisha kwenye maeneo yote ya maisha kupokea mgeuko, lakini bado anamtegemea mwanadamu kutengeneza mazingira hayo
Luka 5:17-21 “Ikawa siku zile mojawapo alikuwa akifundisha, na Mafarisayo na waalimu wa torati walikuwa wameketi hapo, waliotoka katika kila kijiji cha Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu; na uweza wa Bwana ulikuwapo apate kuponya. Na tazama, wakaja watu wanamchukua kitandani mtu mwenye kupooza; wakataka kumpeleka ndani na kumweka mbele yake. Hata walipokosa nafasi ya kumpeleka ndani kwa ajili ya lile kundi la watu, walipanda juu ya dari wakampisha katika matofali ya juu, wakamshusha yeye na kitanda chake katikati mbele ya Yesu. Naye alipoiona imani yao, alimwambia, Ee rafiki, umesamehewa dhambi zako.”
Mungu na ukuu wake wote anaweza kumgusa mtu mmoja kati ya kundi kubwa la watu, mtu huyo lazima yuko tayari kutumia nguvu ya mgeuko huo wa kiungu ambao tayari upo.
Miujiza huwa haiwafuati watu wanaongoja, miujiza inawaendea wanang’ang’ania, wanaotafuta, wanaojituma kuupokea miujiza yao.
- Mazingira ya ufalme yanayosababisha mgeuko wa kiungu huchochewa binafsi na sio kama kundi (Individually provoked )
Mungu hashughuliki na makundi, anashughulika na mtu mmoja mmoja, wakati anataka uamsho utokee kanisani, atamtumia mtu mmoja ambaye anaambukiza wengine uamsho huo. Mungu anamshughulikia mtu mmoja; unapokua mwenyewe katika kumwendea unakidhi vigezo vya kupokea mgeuko wa Kiungu.
Ezekieli 2:1 “Akaniambia, Mwanadamu, simama kwa miguu yako, nami nitasema nawe.”
Muujiza unaoutaka wewe, yamkini mwingine hauhitaji; kila mtu ana uhitaji wa kibinafsi ambao anamtarajia Mungu amtokelezee; hivyo Mungu anamtokezea kila mmoja mmoja pale anapokwenda mwenyewe kibinafsi kwa Mungu.
Matendo 14:10 “akasema kwa sauti kuu, Simama kwa miguu yako sawasawa.
Akasimama upesi akaenda.”
- Mazingira ya mgeuko wa Kiungu yanaweza kuwepo mahali lakini hakuna anayetambua
Yeremia 8:22 “Je! Hapana zeri katika Gileadi? Huko hakuna tabibu? Mbona, basi, haijarejea afya ya binti ya watu wangu?”
Macho ya mwamini yanapaswa kufunguka ili atambue mazingira ya Kiungu yenye nguvu za kuleta mgeuko kwenye maisha. Unaweza kuwa karibu na tiba, na dawa na majibu ya msaada lakini usipoweza kuuona huwezi kusaidika.
Kuna tabia mtu anakua nayo kabla hajajua Mungu yuko mahali, na kuna tabia inatengenezwa kwa upya mtu anapotambua kuwa Mungu yupo, na yupo kuleta mgeuko wa maisha yake
Kazi kubwa ya mwamini, ni kutambua tu nguvu za Mungu zipo, maana ni kweli nguvu za Mungu. Ingawa nguvu za Mungu ziko kila mahali na kwa watu, lakini Mungu anadhihirisha nguvu zake kwa mtu binafsi pale anapozitambua kibinafsi.
Mwanzo 28:16 “Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli BWANA yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni.”
Unapotambua nguvu za Mungu za kuleta mgeuko hatua inayofuta huwa ni thawabu; thawabu huwa zinakwenda zilipotambuliwa.
- Watu hubeba hali ya hewa ya kiroho (watu wana mazingira ya kwao wanayobeba) ya uwepo wa Mungu.
Hali ya hewa ya kiroho aliyoibeba mtu inaweza kusababisha mtu asipokee mgeuko wa Kiungu kwenye maisha yake; mwamini anapaswa kushughulika na hali yake ya kiroho iendane na hali ya uwepo wa mazingira ambayo nguvu za Mungu zipo.
Luka 13:11 “Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa.”
- Nyumba ya Mungu, ni mwenyeji wa nguvu zinazosababisha mgeuko wa kiungu Mtumishi wa Mungu ni chanzo cha kusababisha mgeuko wa kiungu kwenye maisha ya watu, mtumishi wa Mungu sio chanzo, ni chombo cha kuleta mgeuko;
Ezekieli 46:9 “Lakini watu wa nchi watakapokuja mbele za BWANA katika sikukuu zilizoamriwa, yeye aingiaye kwa njia ya lango la upande wa kaskazini ili kuabudu, atatoka kwa njia ya lango la upande wa kusini; na yeye aingiaye kwa njia ya lango la upande wa kusini, atatoka kwa njia ya lango la upande wa kaskazini; hatarudi kwa njia ya lango aliloingia kwalo, lakini atatoka kwa kwenda mbele moja kwa moja.” Jinsi unavyoingia nyumbani mwa Bwana kunakua na mgeuko wa Kiungu.